KOCHA mpya wa Simba, Didier Gomes ameukubali uwezo wa nyota mpya, Mzimbabwe Perfect Chikwende lakini akasema Mnigeria Junior Lokosa anahitaji muda
Kocha mpya wa Simba, Gomes tangu ameanza kazi nchini amesimamia mazoezi ya timu hiyo katika awamu tatu na kutoa mtazamo wake juu ya nyota hao wawili wapya na wachezaji wengine pia.
Gomes alisema kwa jinsi wamefanya mazoezi amebaini kwa upande wa nyota wa kigeni, Chikwende amemfurahisha kwa kufanya vizuri zaidi mara kwa mara katika maeneo mengi.
“Awali nilikuwa namsikia na nilipata muda wa kumfuatilia kwa kuangalia mechi zake za nyuma, lakini baada ya kuwa naye, nimebaini ni moja ya wachezaji bora ambao tumesawajili.”
“Chikwende amekuwa akifanya vizuri katika kila zoezi ambalo tunafanya na ameonyesha ni mchezaji anayependa ushindani na kutamani kucheza zaidi,” alisema Gomes.
Aliongeza “Muda mfupi ambao nimekaa naye nimebaini anaweza kuwa na mpira mguuni na ngumu kupoteza, anapiga pasi nzuri pamoja na kupenda kupiga chenga walinzi wa timu pinzani, akiwa na mpira ana uwezo wa kukimbia pamoja na mengine mengi ambayo nitayabaini kutoka kwake katika siku zijazo
“Lokosa anahitaji muda zaidi wa kufanya mazoezi mbalimbali ili kuwa fiti kimwili kwanza ili kuweza kushindana na wachezaji wa timu pinzani, lakini kuzoea kucheza mpira ili kutimiza majukumu yake ya kufunga,” alisema.
Simba imemalizana pia na Mcongomani, Doxa Gikanjia na amesainishwa mkataba wa miezi sita akiwa katika majukumu ya timu ya taifa ya DR Congo, inayoshiriki mashindano ya Chan, huko nchini Cameroon. Mbali na huyo pia yumo Peter Muduwa ambaye alitarajiwa kutambulishwa jana.
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, Salim Abdallah ‘Try Again’ alifichua wanahitaji kuwa na mawinga wenye maudambwi udambwi kama wa Luis Jose ndio maana wakamsainisha Chikwende.
“Tunahitaji kuwa na mawinga wenye nguvu na mbio kama anvyofanya na Luis na kwa Chikwende ni hatari, subirini ligi ianze mtajua nini tunakimaanisha kuhusu usajili huo.”
“Chikwende ni kama Morisson tu na Simba ya sasa inasajili wachezaji kama hawa ambao watakuwa na tija na umuhimu ndani ya timu na sio ilimradi kusajili tu, tunamleta mtu ambaye anakuwa na faida ndani ya timu, wao wanaongoza ligi lakini nafasi hiyo ni ya kwetu sisi Simba hatuna mzaha kabisa, ubingwa wa Ligi lazima tuutetee na hata FA, huko Ligi ya Mabingwa ndio tunapambana tufike hatua ya juu zaidi,” aliongeza
0 Maoni